Radio Osotua › Local News

Gachagua Awataka Vijana Kuepuka Kumbukumbu ya Maandamano ya Juni 25.

Local News June 23, 2026 John Waicua

Kinara wa chama cha DCP, Rigathi Gachagua, amewataka vijana kutoshiriki katika shughuli za kumbukumbu za waathiriwa wa maandamano ya Juni 25, 2024, zitakazofanyika Alhamisi wiki hii, akidai kuwa kuna njama za kuzua vurugu wakati wa shughuli hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Wamunyoro, Gachagua alisema baadhi ya viongozi serikalini wamepanga mikakati ambayo inaweza kuhatarisha usalama wa wananchi watakaoshiriki shughuli hizo. Alimlaumu Rais William Ruto pamoja na Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen, akidai kuwa wamehusika katika mipango inayoweza kusababisha madhara kwa Wakenya.

Aidha, Gachagua amewataka wafanyabiashara kutofungua biashara zao siku hiyo kama ishara ya mshikamano na waliopoteza maisha wakati wa maandamano ya kupinga serikali mwaka 2024.

Vilevile, alidai kuwa kuna makundi ya vijana waliolipwa ambao huenda wakatumika kuharibu mali na kuzua fujo, hali ambayo inaweza kutoa nafasi kwa maafisa wa usalama kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya wananchi.

Gachagua ametaja kaunti za Mlima Kenya, Nairobi, Kajiado na Narok kuwa miongoni mwa maeneo yanayoweza kushuhudia visa vya vurugu iwapo hatua za tahadhari hazitachukuliwa. Hata hivyo, hajatoa ushahidi wa madai hayo.