Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI imeomba radhi baada ya kukashifiwa kwa kutumia picha zisizo sahihi kuonyesha watu wanaokisiwa kuleta fujo wakati wa maandamano ya siku ya Jumatatu.

Aidha DCI imesukuma sehemu ya lawama kwa wananchi, ikisema, mkanganyiko huo ulitokana na taarifa nyingi walizopokea kupitia mtandao wa #FichuakwaDCI kuhusu matukio ya vurugu yaliyoripotiwa.

Hata hivyo idara hiyo imeendelea kutoa wito kwa umma kwa taarifa kuhusu waliko watuhumiwa hao ambao picha zao zilichapishwa kwenye mtandao wa kijamii.

Baadhi ya picha zilizotumika zilikuwa za maandamano ya hapo awalihuku zingine zikiwa za mwaka 2008 na moja haikuwa hata Kenya.

Katika mojawapo ya picha zinazozungumziwa, waandamanaji wanaonekana kukimbilia usalama huku kukiwa na machafuko, hata hivyo, upekuzi wa picha hiyo unaonyesha kuwa picha hiyo ilitoka kwa maandamano nchini Burundi na ilitumika katika makala ya Al Jazeera mwaka 2015.

March 25, 2023