Radio Osotua › Church Updates

KCCB Yawaalika Wakristu Katika Maombi Ya Kitaifa.

Church Updates September 1, 2026 Brigit Agwenge

Baraza la Maaskofu wa kanisa katoliki nchini (KCCB) limewaalika wakristu na watu wenye nia njema kote nchini kukusanyika katika Shrine ya Subukia Oktoba 3, 2026, kwa Siku ya Maombi ya Kitaifa ya kila mwaka.

Siku ya Maombi ya Kitaifa ya mwaka huu itaadhimishwa chini ya kaulimbiu “Heri waleta amani,” ikiwataka waumini kukubali wajibu wao kama vyombo vya amani, umoja na upatanisho nchini.

Katika mwaliko kwa waumini, Mwenyekiti wa KCCB, askofu mkuu Maurice Muhatia, aliwasihi Wakenya kujiandaa kiroho kwa ajili ya maombi hayo ya kila mwaka, akiyaelezea kama fursa kwa taifa kukusanyika pamoja katika sala na shukrani.

Alibainisha kuwa kauli mbiu ya mwaka huu ni muhimu sana huku Kanisa na nchi zikijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Zaidi ya hayo, aliwasihi Wakenya kutambuana kama watu wa familia moja ya kibinadamu, bila kujali tofauti za kikabila, kisiasa, kijamii au kidini.

Siku ya Maombi ya Kitaifa ya 2026 itaongozwa na Jimbo Kuu Katoliki la Kisumu, likiunganisha majimbo Katoliki ya Lodwar, Kitale, Eldoret, Kapsabet, Bungoma, Kakamega, Homabay, na Kisii, pamoja na Jimbo Kuu la Kisumu.

Askofu Mkuu Muhatia aliwahimiza Wakatoliki kutoka kote nchini kufanya hija kwenda Subukia na kushiriki katika siku hii muhimu, akiielezea kama wakati wa kuinua taifa na watu wake kwa Mungu.

Maaskofu wamesisitiza mara kwa mara jukumu la sala, mazungumzo, haki, upatanisho na uongozi wenye uwajibikaji katika kujenga taifa lenye amani na mshikamano.