Wizara ya Elimu imetangaza kwamba kalenda ya shule ya muhula wa pili haitabadilika licha ya taharuki katika baadhi ya shule humu nchini.
Akitoa taarifa kuhusu hali ya shule za humu nchini, Waziri wa Elimu Julius Ogamba amesema kwamba visa vya taharuki shuleni vimeripotiwa katika shule 204 pekee za upili, huku asilimia 98% ya shule zikiendelea na shughuli kama kawaida.
Aidha Ogamba alisisitiza kwamba likizo fupi ya muhula huu itatekelezwa kama ilivyoratibiwa kuanzia Juni 24 hadi Juni 28, 2026. Vilevile Ogamba ametangaza mikakati ambayo wameweka kama wizara ili kuhakikisha kuwa visa hivyo vya taharuki vinapungua shuleni.
Ogamba alisema kwamba mbali na usumbufu katika baadhi ya shule za upili za bweni, mfumo wa elimu unaendelea vizuri. Shinikizo lilikuwa likiongezeka kwa wizara ya elimu kubadilisha kalenda ya shule na kuwafanya wanafunzi wachukue mapumziko ya mapema ya katikati ya muhula.
Hii ilikuwa baada ya machafuko kuripotiwa katika shule kadhaa za upili ambazo zilichomwa na miundombinu mingine kuharibiwa.
Wazazi wamehimizwa kutumia likizo fupi kuzungumza na watoto wao ili wawe raia wanaowajibika na wanaotii sheria.

