Narok-og_image

Mahakama ya Narok imewaachilia kwa dhamana wazazi wa msichana mmoja mwenye umri wa miaka 15, baada yao kumlazimisha kukeketwa kinyume cha sheria licha ya kuwa mjamzito. Wazazi hao, Dennis Kishoiyan na mkewe Mariciana Kishoyian, walifikishwa mbele ya mahakama ya Narok siku ya Ijumaa na kushtakiwa kwa kumkeketa binti yao tarehe 15 mwezi uliopita, kabla ya kufanikiwa kuokolewa na maafisa wa polisi katika eneo la Olokurto.

katika kikao cha mahakama kilichoongozwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama ya Narok, Phylis Shinyanda, binti huyo, ambaye kwa sasa ana ujauzito wa miezi saba, alitoa ushahidi wa jinsi kitendo hicho kilivyotekelezwa na mamake kwa ushirikiano na watu wengine ambao hawakuwepo mahakamani, huku wazazi wake wakipinga mashtaka dhidi yao. Wazazi hao aidha waliililia mahakama kuwaachilia wakieleza kwamba watoto wao wengine walioachwa nyumbani hawana mlezi.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, mahakama iliamua kuwa Bw. Kishoiyan angeweza kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi 30,000 pesa taslimu au bondi ya shilingi laki 100,000, huku mama wa msichana huyo akiachiliwa kwa dhamana ya bure, lakini akiagizwa kukabidhi kitambulisho chake cha kitaifa kwa mahakama kama masharti ya dhamana.

Kesi hiyo itatajwa tena Agosti 25 mwaka huu, huku binti huyo akiendelea kupata nafuu katika hifadhi ya watoto ya Tasaru.

 

Share the love
August 5, 2023