Kadi za simu

Maafisa wa Polisi katika Mji wa Thika wamefanikiwa kumkamata mshukiwa mmoja anayedaiwa kuwa sehemu ya genge la wahalifu wanaojihusisha na wizi kwa kubadilisha kadi za simu.

Mshukiwa huyo, ambaye ametambuliwa kwa jina la Emmanuel Kiprono, alikamatwa baada ya kujitokeza katika kituo cha huduma za mawasiliano akitaka kubadilisha kadi ya simu kwa kutumia nyaraka za uongo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), tukio hilo la kumkamata mshukiwa lilitokea baada ya Emmanuel Kiprono kujaribu kubadilisha laini ya simu katika kituo cha huduma za mawasiliano. Mara tu baada ya kukamatwa, mshukiwa huyo aliwaongoza maafisa wa polisi hadi kwenye nyumba moja iliyoko Zimmerman, ambapo walifanikiwa kupata simu ya rununu inayotumika kusajili kadi hizo za simu, pamoja na kadi kadhaa za kubadilisha,vitambulisho vya uongo miongoni mwa vifaa vingine alivyotumia.

DCI imethibitisha kuwa mshukiwa huyo ni mmoja wa wahalifu wa kundi ambalo limekuwa likitekeleza uhalifu wa aina hii, hususan katika eneo la Mulot.

Maafisa wa polisi wanatoa wito kwa umma kutoa ushirikiano wao kwa kutoa taarifa zinazoweza kusaidia katika kukabiliana na uhalifu wa aina hii, kwa kutoa taarifa kupitia nambari zao za #FichuaKwaDCI 0800 722 203.

 

Share the love
September 28, 2023