Radio Osotua › Narok County

Mwanamume Afariki Kwa Kupigwa Risasi Baada Ya Kumshambulia Polisi Narok.

Narok County March 30, 2026 Anthony Mintila

Mwanaume mmoja wa umri wa makamo ameuawa kwa kupigwa risasi na afisa wa polisi katika Kituo cha Polisi cha Sakutiek, Narok Kaskazini, kufuatia ugomvi uliozuka kati yao.

Akithibitisha tukio hilo, Chifu wa eneo hilo, Josphat Napikue, amesema kuwa marehemu alifika katika kituo hicho akitaka kumuona ndugu yake aliyekuwa akizuiliwa.

Amesema kuwa hali ilibadilika na kuwa ugomvi, ambapo mwanaume huyo alidaiwa kumshambulia afisa wa polisi kwa kumkata kwa kisu.

Kwa mujibu wa chifu huyo, afisa wa polisi alijibu kwa kufyatua risasi na kumuua mwanaume huyo papo hapo.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti mjini Narok, huku afisa wa polisi akipokea matibabu jijini Nairobi baada ya kujeruhiwa katika tukio hilo.