Sondu - Kisumu Kericho

Rais William Ruto amejitokeza kwa kishindo na kuvunja kimya chake kuhusu suala la machafuko katika eneo la Sondu, mpakani mwa kaunti za Kericho na Kisumu. Akiwahutubia wananchi leo katika eneo la Nyando, Rais Ruto ametoa agizo la kukamatwa na kushtakiwa kwa wale wote wanaohusika na kuvuruga amani katika eneo hilo.

Kiongozi wa taifa ambaye alianza ziara yake ya siku nne katika ukanda wa Nyanza, amesisitiza kwamba wale wote wanaojihusisha na vitendo vya kuleta machafuko na kuharibu amani ya eneo hilo hawatakuwa na nafasi katika taifa la Kenya. Wananchi walimtaka Rais kulizungumzia suala hilo, kabla ya kumaliza hotuba yake baada ya kushuhudia uzinduzi wa ujenzi wa Kituo cha Uvuvi cha Kabonyo. Kiongozi wa taifa alisema tayari agizo limetolewa kwa waziri wa usalama wa ndani.

“Niwahakikishie ya kwamba kila mtu ambaye alisababisha mwananchi akapoteza maisha yake lazima akamatwe na apelekwe jela” Rais William Ruto

Kando na operesheni ya usalama katika eneo hilo, pia alieleza kwamba kuna mipango ya uzinduzi wa miradi ya maendeleo.

SOMA PIA: Watu wanne waaga dunia katika mapigano Sondu

Ziara ya Rais katika ukanda wa Nyanza imejumuisha ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika kaunti za Kisumu na Siaya. Viongozi wa kisiasa katika eneo hilo, akiwemo Gavana Prof. Anyang’ Nyongo wa Kisumu na Gavana James Oreng’o wa Siaya, walimkaribisha rais na kuahidi ushirikiano.


 

Share the love
October 6, 2023