Radio Osotua › Narok County

Serikali Yashinikizwa Kuingilia Kati Bei ya Mafuta Narok

Narok County March 28, 2026 John Waicua

Wahudumu wa boda boda na teksi mjini Narok wameitaka serikali kuingilia kati ili kudhibiti bei ya mafuta, wakionya kuwa ongezeko la bei litawaathiri pakubwa katika shughuli zao za kila siku.

Wakizungumza na wanahabari, wahudumu hao walisema kuwa kumekuwa na tabia ya baadhi ya wauzaji wa mafuta kupandisha bei kiholela kila kunapozuka taarifa za upungufu wa mafuta nchini. Aidha, walidai kuwa baadhi ya wafanyabiashara huficha mafuta kwa makusudi ili baadaye wauze kwa bei ya juu zaidi.

Wafanyabiashara hao pia wameitaka serikali kupunguza ushuru na ada mbalimbali zinazotozwa bidhaa za mafuta, wakisema hatua hiyo itasaidia kushusha gharama na hivyo kuwanufaisha watumiaji wa kawaida.

Wakati huo huo, wauzaji wa bidhaa za kitalii wameeleza wasiwasi wao kuhusu hali ya kisiasa ya kimataifa, wakitaka kusitishwa kwa mivutano inayoendelea kati ya Marekani na Israeli dhidi ya Iran. Wamesema kuwa hali hiyo inaweza kuathiri uchumi wa Kenya, hasa ikizingatiwa utegemezi wa nchi kwa bidhaa kutoka mataifa hayo.

Wafanyabiashara hao wameonya kuwa endapo hali hiyo itaendelea, huenda gharama za maisha zikapanda zaidi na kuathiri sekta mbalimbali za uchumi nchini.