Radio Osotua › Local News

Wanafunzi 16 Wafariki Kwenye Mkasa Wa Moto.

Local News May 28, 2026 Brigit Agwenge

Wanafunzi kumi na sita wamethibitishwa kufariki kufuatia mkasa wa moto katika shule ya Wasichana ya Utumishi huko Gilgil, Kaunti ya Nakuru, huku polisi wakisema wanafunzi wengine kadhaa wamelazwa hospitalini wakiwa na majeraha.

Kwa mujibu wa Polisi ni kwamba wanafunzi 74 wamelazwa hospitalini baada ya tukio hilo, ambalo liliripotiwa mapema Alhamisi.Katika ripoti ya tukio iliyowasilishwa katika Kituo cha Polisi cha Gilgil, polisi walisema mkuu wa shule, Joycelene Muraguri, aliripoti moto huo mwendo wa saa 4:30 asubuhi.

Bweni lililoathiriwa, lililotambuliwa kama Meline Waithera, lilikuwa na wanafunzi 220, wanaojumuisha gredi ya 10, kidato cha 3 na kidato cha 4.

Timu ya mashirika mbalimbali yalishirikiana ili kudhibiti moto huo hata ingawa kiwango cha uharibifu wa mali hakijabainika.

Wale waliojeruhiwa walipelekwa katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Gilgil na Hospitali ya St Mark’s huku polisi wakielezea kama majeraha ya viwango tofauti.

Chanzo cha moto huo hakijabainika kufikia Alhamisi asubuhi.