Wazazi wa wanafunzi waliofariki baada ya kula chakula kilichokuwa na sumu katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Mukumu watapokea Ksh.400, 000 kila mmoja kama fidia kutoka kwa serikali.

Haya ni kulingana na Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu ambaye aliambia Seneti kwamba serikali itatumia Ksh 1.2M kuwafidia wazazi wa wanafunzi 3 walioangamia kutokana na kisa hicho.

Akijibu swali la Seneta wa Kakamega Bonny Khakwale, Machogu hata hivyo alisema baada ya uchunguzi, serikali haitafungua mashtaka yoyote ya jinai dhidi ya aliyekuwa mkuu wa shule hiyo Fridah Ndolo au wasimamizi wa shule.

Aliwaambia Maseneta hao kwamba timu ya mashirika mengi iliyochunguza tukio hilo haikupata hatia yoyote kwa upande wa usimamizi wa shule hiyo.

Machogu alidai kuwa hadi sasa, hakuna ushahidi kwamba ni mwalimu mkuu ambaye alikuwa akisambaza chakula shuleni ili kuwawezesha kumtoza.

May 31, 2023