Ababu Namwamba

Waziri wa Michezo nchini, Ababu Namwamba, anatarajiwa kujiwasilisha bungeni adhuhuri ya leo, ili kujibu maswali kutoka kwa wabunge, hususan baada ya kuibuka kwa madai ya utumizi mbaya wa ofisi yake. Baadhi ya maswala ambayo Waziri Namwamba anatarajiwa kujibu ni pamoja na jukumu la Wizara yake katika kuisaidia timu ya Kenya iliyohudhuria Michezo ya Olimpiki ya watu wenye mahitaji maalum iliyofanyika Berlin, Ujerumani mwezi Juni.

Aidha, wabunge pia wanatarajiwa kumuuliza Waziri huyu maswali kuhusu mapokezi ya wanariadha na wanamichezo wengine wanaorejea nchini baada ya kuliwakilisha taifa. Waziri Namwamba ametakikana kujiwasilisha bungeni baada ya kuibuliwa kwa tuhuma za uongozi usiofaa zilizotolewa na Mbunge wa Kikuyu, Kimani Ichungwah, na Seneta wa Nandi, Simon Cherargai.

Kikao hiki cha bunge kinatarajiwa kuwa na mjadala mkali huku wabunge wakijaribu kuchunguza masuala yanayohusiana na utendaji wa Wizara ya Michezo na mchango wake katika maendeleo ya michezo nchini Kenya. Waziri Namwamba atakuwa na jukumu la kutoa maelezo na kujibu maswali ya wabunge ili kutoa ufafanuzi kuhusu masuala yote yanayohusiana na Wizara yake.

 

Share the love
August 23, 2023