Mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro, ameonya kuwa Kenya iko kwenye hatari ya kushindwa kulipa madeni yake na kudhoofika kiuchumi, iwapo serikali itaendelea na mwenendo wa sasa wa matumizi ya kiholela na ukopaji usio na mpango.
Akizungumza wakati wa kongamano la Taasisi ya Fedha ya Umma lililofanyika katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Nairobi, Nyoro alitoa wito wa kukaguliwa upya kwa mchakato wa kutunga bajeti ya taifa. Alisema kuwa gharama za mara kwa mara zimepanda kupita kiasi, hali inayonyima sekta ya maendeleo fedha muhimu.
Kwa mujibu wa Nyoro, zaidi ya Ksh1.25 trilioni ya bajeti ya kila mwaka hutumika katika gharama zisizobadilika kama mishahara, masurufu na ulipaji wa riba ya madeni, huku kiasi kinachotengwa kwa miradi ya maendeleo kikizidi kupungua.
“Tunajiandaa kwa msimu mwingine wa uchaguzi na kuna uwezekano mkubwa wa Tume ya Uchaguzi kuwasilisha ombi la zaidi ya Ksh60 bilioni—kiasi ambacho ni kikubwa kuliko kinachotolewa kwa sekta nzima ya barabara,” alisema Nyoro, ambaye pia ni mwenyekiti wa zamani wa Kamati ya Bajeti katika Bunge la Taifa.
Aliongeza kuwa hali hii inazidi kuzorotesha uwezo wa serikali kutoa huduma bora kwa wananchi na kutekeleza miradi ya maendeleo kama ujenzi wa shule, hospitali na barabara.
Mbunge huyo pia alisisitiza haja ya kufanyiwa marekebisho ya kitaasisi ili kuongeza ufanisi serikalini. Alisema Kenya inaweza kupunguza ukubwa wa serikali bila kudhoofisha utoaji wa huduma, akieleza kuwa hatua hiyo itaongeza tija na kupunguza mzigo wa matumizi.
Kauli yake inajiri wakati ambapo Wizara ya Hazina ya Kitaifa inajiandaa kuwasilisha makadirio ya bajeti ya mwaka ujao wa kifedha, huku mjadala mkubwa ukiibuka kuhusu jinsi ya kusawazisha majukumu ya kikatiba, ulipaji wa madeni, na mahitaji yanayoongezeka ya maendeleo ya umma.