Kamati ya Fedha katika Bunge la Kitaifa imependekeza kuondolewa kwa kifungu kinachozua utata kwenye mswada wa Fedha wa mwaka 2025, ambacho kingeipa Mamlaka ya ukusanyaji wa Mapato nchini (KRA) uwezo wa kufikia taarifa za kibinafsi na za kifedha za wakenya.
Kifungu hicho kilikuwa kinapendekeza kufutwa kwa kipengele cha sheria ambacho kinazuia KRA kuwalazimisha wafanyabiashara kutoa taarifa za kibinafsi za wateja wao. Ikiwa kifungu hicho kingepitishwa, KRA ingeruhusiwa kufikia taarifa kama vile miamala ya pesa kupitia simu na benki, pamoja na siri za kibiashara, bila masharti, hatua ambayo KRA inasema inalenga kudhibiti ukwepaji wa ushuru.
Hata hivyo, kamati hiyo imebaini kuwa mapendekezo hayo hayakidhi matakwa ya Katiba kuhusu haki ya faragha na huenda yakachochea uwezekano wa matumizi mabaya ya taarifa za binafsi, usalama wa data na ukiukaji wa haki za raia. Kamati pia imeeleza kuwa sheria zilizopo tayari zinaipa KRA uwezo wa kufuatilia taarifa za kifedha kwa njia ya kisheria, ikiwa ni pamoja na kupata kibali cha mahakama, jambo linalowezesha ufuatiliaji unaozingatia sheria.
Taarifa ya kamati hiyo ambayo itawaslishwa katika vikao vya bunge, imeonyesha kuwa kulinda faragha ya wananchi na kuheshimu taratibu za kisheria ni muhimu katika kujenga imani ya wakenya na kuhakikisha viwango vya kimataifa vya ulinzi wa taarifa binafsi.
Licha ya upinzani mkubwa kutoka kwa wadau mbalimbali, Wizara ya Hazina ya Taifa imeendelea kutetea pendekezo hilo, ikilieleza kama hatua muhimu ya kuongeza ufanisi wa ukusanyaji ushuru. Takwimu kutoka KRA zinaonesha kuwa kati ya Wakenya milioni 20 walio na nambari ya utambulisho wa ushuru (KRA PIN), ni milioni 10 pekee wanaowasilisha marejesho ya ushuru, huku milioni sita kati yao wakiripoti kutopata mapato kabisa.