IEBC Mahakama

    Jopo la majaji watatu linatarajiwa kutoa uamuzi leo mchana kuhusu hatua ya Rais William Ruto kuwateua maafisa wa IEBC licha ya kuwepo kwa agizo la Mahakama la kuzuia uteuzi huo.

    Uamuzi huu unatarajiwa hii leo, baada ya kikao cha jana kuahirishwa bila uamuzi kutolewa. Katika kikao hicho, wakili Paul Muite ambaye ni mmoja wa walalamishi katika kesi hiyo alieleza kuwa Bunge la Kitaifa halikuwa na uwezo wa kikatiba wa kuwapiga msasa makamishna hao. Alidai kuwa bunge hilo, likiongozwa na Spika Moses Wetang’ula, limekuwa na mapendeleo na linakosa uhuru wa kweli katika kutekeleza majukumu yake.

    Mahakama ilikuwa tayari imetoa amri ya muda ya kuzuia uteuzi, kuchapishwa kwa majina, au kuapishwa kwa makamishna wa IEBC waliopigiwa msasa na Bunge. Hata hivyo, mapema mwezi huu, Rais alichapisha notisi rasmi ya uteuzi wa makamishna hao katika gazeti la serikali, hatua ambayo imezua mvutano wa kisheria.

    Walioorodheshwa katika notisi hiyo ni mwenyekiti Erastus Edung Ethekon na makamishna Ann Njeri Nderitu, Moses Alutalala Mukhwana, Mary Karen Sorobit, Francis Odhiambo Aduol, Hassan Noor Hassan na Fahima Arafat Abdallah.

    Uamuzi wa majaji hao unatarajiwa kutoa mwelekeo wa kisheria kuhusu iwapo hatua ya Rais ilikiuka mamlaka ya mahakama na katiba ya nchi.

    June 24, 2025