Mchuuzi Boniface Kariuki, aliyepigwa risasi na afisa wa polisi tarehe 17 Juni na baadaye kuaga dunia, anatarajiwa kuzikwa leo katika eneo la Kangema, Kaunti ya Murang’a.
Familia ya Kariuki iliandaa ibada ya wafu siku ya Jumatano huku ikiendelea kushinikiza haki dhidi ya afisa wa polisi anayetuhumiwa kuhusika katika mauaji hayo.
Wakati maandalizi ya mazishi yakiendelea, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) imetangaza kuanzisha kesi ya mauaji dhidi ya afisa wa polisi Barasa Masinde, ambaye alinaswa kwenye kamera akimpiga risasi Kariuki na kusababisha kifo chake. Hata hivyo, afisa mwingine aliyehusishwa na tukio hilo Duncan Kiprono, aliachiliwa huru.
Kariuki alifariki mapema mwezi huu akiwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) ambapo alikuwa amelazwa na kufanyiwa upasuaji wa ubongo kutokana na majeraha aliyoyapata.