Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, ametoa wito kwa wanaomiliki bunduki haramu pamoja na washukiwa wa ujambazi katika Bonde la Kerio kujisalimisha. Amewataka wafanye hivyo mara moja ili kulinda usalama wao binafsi na wa jamii kwa jumla.
Akizungumza akiwa katika kikao cha Jukwaa la Usalama katika kaunti ya Elgeiyo Marakwet, Murkomen amesema serikali imejitolea kuhakikisha kuwa wahalifu wote wanakamatwa. Kwa mujibu wa Waziri, baadhi ya washukiwa tayari wamekamatwa. Wengine waliokuwa wakipinga kukamatwa wameuawa kwenye makabiliano na polisi. Aliwaeleza waandishi wa habari kuwa waliobaki sasa wako mafichoni pangoni na kwenye maeneo ya milimani.
“Tunafanya kila juhudi kuwanasa wahalifu hawa,” alisema Waziri. “Baadhi yao wana wafuasi, na baadhi ya washirika wao tayari wamekamatwa. Waliosalia wamekimbilia mafichoni, na hii ndiyo sababu sehemu za Bonde la Kerio zinaonekana tulivu kwa sasa.”
Murkomen pia aliwashutumu vikali baadhi ya watu wenye ushawishi katika maeneo ya Kapsawar, Eldoret, Iten na Trans Nzoia kwa kuwasaidia wahalifu hao. Alieleza kuwa baadhi yao wamekuwa wakiwahifadhi majambazi kwa siri, huku wengine wakihusika katika biashara haramu ya silaha na risasi.
Waziri alifichua kuwa baadhi ya “wataalamu” na watu wenye hadhi kijamii wamekuwa wakitumiwa kama sehemu ya mtandao wa kuwapa wahalifu hifadhi salama, hasa wakati wa operesheni za polisi.
“Wako waliokuwa wanahifadhi majambazi Kapsawar. Wengine wako Eldoret na Iten. Kuna pia wanaoendesha shughuli hizi kutoka Trans Nzoia. Wote hawa wameshiriki kwa njia moja au nyingine. Wengine huuza risasi na wengine hutoa msaada wa kifedha. Natoa wito wajisalimishe haraka,” alisema Murkomen.
Waziri huyo alisisitiza kuwa serikali haitawavumilia wale wanaowasaidia wahalifu kwa njia yoyote ile. Alisema kila mtu anayehusika atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Aliwataka wananchi wa Bonde la Kerio kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa muhimu zitakazosaidia kukomesha kabisa vitendo vya uhalifu.
“Wananchi wana nafasi muhimu sana katika kudumisha amani. Tukishirikiana, tunaweza kuhakikisha usalama wa kudumu katika eneo hili,” aliongeza.