Watu 2,933 wameaga dunia kati ya Januari na tarehe 10 Agosti mwaka huu kutokana na ajali za barabarani, kwa mujibu wa Wizara ya uchukuzi nchini. Kati yao, 80 walipoteza maisha ndani ya siku nne pekee zilizopita.

    Ajali hizi zimehusisha magari ya abiria, magari binafsi na malori ya biashara. Hali hii imeongeza hofu kuhusu utekelezaji wa sheria za usalama barabarani. Waziri wa Uchukuzi, Davis Chirchir, amesikitikia ongezeko hili na kuwataka watumiaji wote wa barabara kuzingatia kanuni za usalama kwa umakini na uwajibikaji.

    Serikali imetangaza kuunda jopo maalum litakalofanya ukaguzi wa usalama katika maeneo yanayojulikana kwa ajali mara kwa mara. Jopo hilo litahusisha maafisa kutoka mashirika mbalimbali ya serikali na sekta binafsi. Watachunguza maeneo hatarishi, kubaini mapungufu ya usalama, na kutoa mapendekezo ya hatua za kuzuia ajali. Tathmini hiyo inatarajiwa kukamilika ndani ya siku saba, kisha hatua za kuokoa maisha zitaanza mara moja.

    Aidha, Wizara imesisitiza kuwa Mpango wa Kitaifa wa Usalama Barabarani 2024–2028 utaendelea kutekelezwa. Mpango huu unalenga kudhibiti ulevi miongoni mwa madereva, kuimarisha usalama wa usafiri wa shule, kufanya ukaguzi wa magari na vituo vya kando ya barabara, pamoja na kupitia upya sheria za trafiki ili kuongeza usalama wa watumiaji wote wa barabara.

    Waziri Chirchir pia amewapongeza NTSA kwa juhudi zake za kuendeleza elimu ya umma kuhusu usalama barabarani. Amehimizwa madereva, waendesha bodaboda, waendesha baiskeli na watembea kwa miguu kufuata sheria kikamilifu. Amesisitiza kuwa ajali nyingi zinaweza kuzuilika ikiwa kila mtumiaji wa barabara atatimiza wajibu wake.

    August 12, 2025

    Leave a Comment