Tarehe 10 Novemba 2025 Kanisa Katoliki nchini liligubikwa na huzuni kufuatia taarifa za kifo cha Askofu Mstaafu Philip Sulumeti. Katika kukumbuka urithi wake, tunatazamia safari ya maisha yake, imani, uongozi na mchango wake kwa Kanisa na Taifa.

    Maisha ya Utotoni

    Philip Sulumeti alizaliwa tarehe 5 Agosti 1937 katika kijiji cha Kotula, Ankura, kaunti ya Busia. Alikuwa mtoto wa familia ya kawaida ya kijijini, na hakuna aliyetabiri angekuja kushika nafasi za juu Kanisani akiwa mdogo. Tarehe 28 Agosti mwaka huo huo, alipokea sakramenti ya ubatizo kutoka kwa Padre Thomas. Elimu yake ilianzia Shule ya Msingi ya Ankura kati ya 1946 na 1951. Baadaye alijiunga na Seminari ya St. Peter’s Mukumu kuanzia 1952 hadi 1958 kwa elimu ya upili.

    Safari ya Masomo ya Kiroho

    Baadaye alitumwa kuendeleza masomo ya falsafa katika Seminari ya Gaba nchini Uganda kati ya 1959 na 1960, kisha akarejea hapo hapo kuanzia 1961 hadi 1965 kusomea teolojia. Wito wake ulizidi kudhihirika na kukomaa, na tarehe 29 Juni 1965 aliwekwa wakfu kuwa shemasi. Mwaka wa 1966, akiwa na umri wa miaka 28, alipokea daraja takatifu la upadre katika Parokia ya Central Siuma, Ankura.

    Huu ulikuwa ni wakati ambapo Kanisa Katoliki nchini Kenya lilikuwa linaanza kukabidhi uongozi kwa makleri wazawa, na pia lilikuwa linaanza kuakisi utamaduni na ladha ya Kiafrika katika ibada na maisha ya kiroho. Akiwa kijana mwenye bidii na kipaji kikubwa, Sulumeti alipata nafasi adimu ya kwenda Roma kujiendeleza zaidi. Alihudhuria Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana ambako alihitimu katika sheria za Kanisa (Canon Law), na hivyo kuwa miongoni mwa wataalam wachache waliobobea katika taaluma hiyo nchini.

    Uwezo wake wa uongozi na umahiri wake katika kazi za Kanisa vilidhihirika mapema. Mwaka 1972, akiwa na umri wa miaka 35 tu, aliteuliwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Kisumu, akihudumu chini ya Askofu Joannes de Reeper. Baada ya miaka minne, mwaka 1976, aliteuliwa kuwa Askofu wa Kisumu kufuatia kustaafu kwa Askofu de Reeper, na hivyo kuwa Askofu wa kwanza Mwafrika kuongoza jimbo hilo.

    Ukuaji wa Kanisa na Huduma kwa Jamii

    Ukuaji wa kasi wa Kanisa katika eneo la magharibi mwa Kenya ulichochea kugawanywa kwa Jimbo la Kisumu mwaka 1978. Jimbo la Kakamega lilizaliwa na Sulumeti aliteuliwa kuwa askofu wake wa kwanza akiwa na umri wa miaka 40. Askofu Zacchaeus Okoth alichukua hatamu za Jimbo la Kisumu. Katika Jimbo la Kakamega, alihudumu kwa miaka 37 mfululizo hadi alipostaafu tarehe 5 Disemba 2014 na kupewa cheo cha Askofu mstaafu (Emeritus).

    Katika kipindi chake cha uongozi, Askofu Sulumeti alisimamia ukuaji mkubwa wa Kanisa. Alianzisha zaidi ya parokia 40 ambazo nyingi zilikuja kujisimamia zenyewe, na alitoa kipaumbele kwa sekta ya elimu akiamini kuwa shule ni msingi wa ujenzi wa jamii yenye mwanga. Chini ya uongozi wake, shule nyingi zilianzishwa na kuimarishwa, huku akipigania kwa nguvu zote elimu ya mtoto wa kike. Upendo wake kwa ustawi wa jamii pia ulijidhihirisha katika kusaidia kuimarisha hospitali mbalimbali katika eneo la Magharibi.

    Mchango Wake Katika Taifa

    Jina lake halikujulikana tu ndani ya kanisa, bali pia katika nyanja za kitaifa. Alihusika katika kuimarisha taasisi muhimu kama Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Masinde Muliro. Aidha, mwaka 2004, alipewa jukumu nyeti la kuongoza kamati ya upatanisho kutafuta mwafaka wa kisiasa uliolenga kuandika Katiba mpya. Ingawa ripoti ya kamati hiyo ilitupiliwa mbali, mchango wake uliendelea kuheshimiwa kama jitihada ya kutafuta umoja wa kitaifa.

    Malezi ya Makleri na Viongozi wa Kanisa

    Katika Kanisa, alilea makleri na viongozi wengi walioendelea kupokea majukumu makubwa. Ni chini ya uongozi wake ndipo makasisi kadhaa walipandishwa cheo, wakiwemo Askofu Mark Kadima wa Bungoma aliyewekwa wakfu kuwa padre mwaka 1993, Askofu Joseph Obanyi Sagwe wa Kakamega, Askofu Mkuu Zacchaeus Okoth, Askofu Longinus Atundo na Askofu Mkuu Maurice Muhatia. Haya yote yalionesha uwezo wake wa kuona mbali na kujenga Kanisa imara kwa siku zijazo.

    Askofu Mstaafu Philip Sulumeti ataendelea kukumbukwa kama kiongozi aliyekuwa mpole, mwaminifu, na mwenye kujitoa kikamilifu katika kazi ya Bwana. Maisha yake yaliigusa mioyo, yakaandika historia katika kanisa na jamii, na yakabaki kuwa alama ya imani, hekima na utumishi.

    Mwenyezi Mungu amjalie mtumishi wake pumziko la amani milele. Amina.

    November 21, 2025

    Leave a Comment