Muungano wa Umoja wa Afrika (AU) umepinga na kulaani juhudi zozote za kuitambua Somaliland kama taifa huru, ukisisitiza kuwa eneo hilo bado ni sehemu ya Jamhuri ya Shirikisho la Somalia.
Katika taarifa iliyotolewa Ijumaa, Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf, amesema msimamo wa AU haujabadilika na unazingatia misingi ya kisheria ya muungano huo tangu kuanzishwa kwake.
Youssouf amesema AU imefuatilia kwa wasiwasi mkubwa mijadala ya hivi karibuni kuhusu hadhi ya Somaliland, akibainisha kuwa muungano huo unakataa kabisa hatua au mpango wowote wa kuitambua kama nchi huru.
Ameonya kuwa jaribio lolote la kubadili mipaka ya Somalia inayotambuliwa kimataifa linakiuka kanuni za Umoja wa Afrika na linaweza kusababisha kuyumba kwa amani na uthabiti barani Afrika.
Kauli ya AU imekuja wakati Israel ilipotangaza kuwa nchi ya kwanza kuitambua rasmi Somaliland kama taifa huru, huku ikieleza nia ya kupanua ushirikiano na eneo hilo katika sekta za kilimo, afya na teknolojia.

