Sikukuu ya Familia Takatifu Yaadhimishwa Duniani
Kanisa Katoliki duniani hii leo linaadhimisha Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Kwa mujibu wa taratibu za Kanisa, sikukuu hii huadhimishwa kila Jumapili ya kwanza baada ya Krismasi, au tarehe 30 Desemba endapo Krismasi itaangukia siku ya Jumapili.
Sikukuu hii inalenga kuonyesha Familia Takatifu ya Nazareti kama mfano wa kuigwa na familia za Kikristo kote duniani. Kanisa linawahimiza waumini kuiga maadili ya upendo, uvumilivu, mshikamano na uaminifu, huku changamoto walizopitia Yesu, Maria na Yosefu zikitumika kuwapa faraja wakristo wanaokabiliwa na matatizo ya kifamilia na malezi ya watoto.
Papa Leo wa Kumi na Nne Atoa Msaada kwa Waathiriwa wa Vita Ukraine
Baba Mtakatifu Papa Leo wa Kumi na Nne ameendelea kuonyesha mshikamano wa Kanisa kwa kutoa msaada wa kibinadamu kwa familia zilizoathirika na vita nchini Ukraine. Kupitia Vatican, Papa ametuma malori matatu yaliyobeba zaidi ya pakiti laki moja za chakula maalum ambacho, kwa kuongeza maji, hubadilika kuwa supu yenye virutubisho vya kuku na mboga.
Kwa mujibu wa Kardinali Konrad Krajewski, msaada huo ni ishara muhimu kwa familia zilizolazimika kukimbia makazi yao kutokana na vita. Ameeleza kuwa msaada huo unaonyesha ukaribu wa Papa kwa wakimbizi na wote wanaoishi katika hofu, tabu na mazingira magumu. Pia, Papa amekuwa akituma misaada ya kifedha kwa nchi mbalimbali kupitia ofisi ya misaada ya Vatican hata kabla ya Sikukuu ya Krismasi.
Mlango wa Jubilee Wafungwa katika Kanisa Kuu la Laterano, Roma
Huku siku za mwisho za Mwaka wa Jubilee zikijongea kwa kasi januari 6 mwaka ujao, mlango wa Jubilee ulifungwa hapo jana katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yohane Laterano mjini Roma. Ibada ya kufunga mlango huo iliongozwa na Kardinali Baldassare Reina, Vicar General wa Roma na Mkuu wa Kanisa hilo.
Kabla ya kuufunga mlango huo, Kardinali Reina alipiga magoti na kusali kimya kimya, tukio lililowagusa waumini wengi waliohudhuria. Baada ya mlango kufungwa, waumini walikaribia kizingiti cha mlango huo kwa sala na tafakari. Katika mahubiri ya Misa iliyofuata, Kardinali Reina aliwahimiza waumini kuwa mashahidi wa imani kwa kuonyesha undugu, haki, ukweli na amani, akisisitiza kuwa imani ya Kikristo haiwezi kuishi bila kuwajali wanaoteseka na waliokata tamaa katika maisha.
