Askofu Willybard Kitogho Lagho

    Askofu Willybard Kitogho Lagho wa Jimbo Katoliki la Malindi ameteuliwa na Baba Mtakatifu Papa Leo XIV kuwa mjumbe wa Dikasteri ya Vatican ya Majadiliano ya Kidini (Dicastery for Interreligious Dialogue).

    Vatican ilitangaza uteuzi huu siku ya Alhamisi tarehe 3 Julai. Askofu Lagho ataungana na viongozi wengine kusaidia Kanisa katika kutekeleza jukumu lake la kukuza majadiliano na ushirikiano na dini zingine.  kwa ajili ya kudumisha amani na mshikamano duniani.

    Askofu Lagho, ambaye aliteuliwa kuwa Askofu wa Malindi mwaka 2020, alizaliwa tarehe 23 Machi 1958, Taita-Taveta, ndani ya Jimbo Kuu la Mombasa. Alisoma falsafa katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Augustine, Mabanga (1980–1982) na theolojia katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Thomas Aquinas, Nairobi (1982–1986), na alipewa daraja takatifu la upadre tarehe 25 Aprili 1997.

    Pia anashikilia Shahada ya Uzamili ya Masomo ya Kidini kutoka Chuo Kikuu Katoliki Afrika Mashariki (CUEA) na Licentiate katika masomo ya Kiarabu na Kiislamu aliyoipata Cairo na katika Taasisi ya Kipapa ya Masomo ya Kiarabu na Kiislamu (PISAI) Roma. Kwenye huduma yake, amewahi kuwa paroko, mlezi wa seminari, mkurugenzi wa vijana na miito, na vika jenerali wa Jimbo Kuu la Mombasa.

    Kwa sasa, Askofu Lagho anahudumu kama Mwenyekiti wa Tume ya Majadiliano ya Kidini na Umoja wa Kikristo (CIRDE) katika Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya (KCCB), na pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Dini Mbalimbali humu nchini (IRCK)

    July 4, 2025

    Leave a Comment