Askofu wa Jimbo Katoliki la Embu, Mhashamu Peter Kimani, ameipongeza serikali kwa kutekeleza Sheria mpya ya matumizi ya Kompyuta na uhalifu wa Mitandaoni, akisema hatua hiyo itasaidia kukuza maadili na matumizi bora ya mitandao ya kijamii nchini.
Akizungumza katika Misa ya Shukrani iliyofanyika katika Chuo cha Embu, Askofu Kimani alisema matumizi mabaya ya mitandao yameongezeka na kuchangia kuporomoka kwa maadili pamoja na kuongezeka kwa lugha za matusi na udhalilishaji.
Amesema kuwa licha ya kuwepo uhuru wa kujieleza, baadhi ya watumiaji wa mitandao wamekuwa wakitumia vibaya nafasi hiyo kusambaza taarifa za uongo, kuchochea chuki na kugawanya jamii. Ameongeza kuwa uhuru huo haupaswi kuumiza wengine wala kuharibu jina la mtu.
Askofu Kimani amewataka vijana kuwa na uwajibikaji wanapotumia mitandao, wakizingatia ukweli, heshima na upendo, kwa kuwa mtandao sasa ni sehemu muhimu ya maisha ya kila siku.
Hata hivyo, ameisihi serikali na mamlaka husika kuhakikisha sheria hiyo inatekelezwa kwa haki bila kukiuka uhuru wa kutoa maoni kwa njia ya haki na ya kujenga.

