Faith Odhiambo

    Rais wa Chama cha Wanasheria LSK Faith Odhiambo, amejiuzulu kama Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Wataalamu lililoundwa kushughulikia fidia kwa waathiriwa wa maandamano. Odhiambo ametaja Muda na amri ya mahakama kama changamoto zilizokwamisha utekelezaji wa majukumu ya jopo hilo.

    Odhiambo amesema uamuzi huo umetokana na kusitishwa kwa shughuli za jopo na mahakama. Aidha, amesema ugumu wa kukamilisha kazi ndani ya muda wa siku 120 uliotolewa umeathiri utendaji. Kwa sasa, waathiriwa wengi wa ukatili wa polisi bado wanahangaika kutafuta haki, jambo linaloashiria kuwa malengo ya jopo hilo huenda hayatafanikiwa kwa wakati.

    Rais huyo vilevile amesema jopo hilo, lililoundwa kupitia tangazo la serikali tarehe 25 Agosti 2025, lilikuwa fursa muhimu ya kuboresha mfumo wa fidia kwa waathiriwa wa ukatili wa polisi na maandamano ya umma. Hata hivyo, kutokana na changamoto za muda na vizuizi vya kisheria, ameamua kuelekeza juhudi zake kupitia uongozi wa LSK. Lengo lake ni kuhakikisha waathiriwa wanapata haki kupitia mfumo wa mahakama.

    Kwa upande mwingine, Odhiambo amesema mawakili wa LSK katika Kisumu tayari wanawakilisha waathiriwa wa ukatili wa polisi mahakamani. Amesema chama hicho kitaendelea kushirikiana na mahakama ili kuharakisha kesi zinazohusiana na ukatili huo. Pia ameeleza kuwa LSK itashirikiana na taasisi za haki na mashirika ya kutetea haki za binadamu kuandaa sheria mpya zitakazorahisisha mfumo wa fidia kwa waathiriwa.

    Kwa mujibu wa taarifa yake, mapendekezo hayo mapya yanalenga kujenga mfumo wa haki unaomweka mwathiriwa katikati ya mchakato wa fidia na kuhakikisha haki inapatikana bila ucheleweshaji.

    Odhiambo amehitimisha kwa kusisitiza kuwa ataendelea kupigania haki za waathiriwa wa ukatili wa polisi na maandamano, akiahidi kuwa LSK itaendelea kusimama na waathiriwa hadi pale haki itakapopatikana.

    October 6, 2025

    Leave a Comment