Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ametangaza kuwa vikosi vya nchi hiyo vimefanikiwa kumuua Mohammed Sinwar, kiongozi mkuu wa Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Akizungumza bungeni (Knesset) Jumatano, Netanyahu alisema Sinwar aliuawa katika shambulio la anga lililolenga Hospitali ya Ulaya mjini Khan Younis, lililotekelezwa Mei 13.
Kwa mujibu wa maelezo ya awali kutoka kwa vyanzo vya Israel, shambulio hilo lilikuwa na lengo mahsusi la kumlenga Sinwar, ambaye ni kaka wa aliyekuwa kiongozi wa Hamas Yahya Sinwar. Yahya aliuawa mwaka 2024 katika shambulio la anga la Israel, na anatajwa kuwa mpangaji mkuu wa mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7, 2023 yaliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 1,200 na utekaji nyara wa wengine zaidi ya 250.
Kifo cha Mohammed Sinwar kinajiri ikiwa ni siku 600 tangu kuanza kwa vita kati ya Israel na Hamas. Tangu wakati huo, Israel imewaua viongozi kadhaa waandamizi wa Hamas, wakiwemo Mohammed Deif—aliyekuwa kiongozi wa kijeshi wa kundi hilo—na Ismail Haniyeh, kiongozi wa kisiasa wa zamani wa Hamas.
Hadi wakati w akuandaliwa kwa taarifa hii, Hamas bado haijatoa tamko lolote kuhusu madai ya Netanyahu.