Kanisa katoliki nchini lmepata jimbo mpya hivi leo, na hii ni baada ya Kiongozi wa kanisa katoliki nchini Papa Francis kuinua hadhi ya Vikariate (Vicarate) ya Kitume ya Isiolo kuwa jimbo katoliki la Isiolo.

Katika tangazo lililochapishwa kwenye mtandao wa kikatoliki wa L’Osservatore Romano adhuhuri ya leo, Baba Mtakatifu Francis pia alimteua Padre Anthony Ireri Mukobo kama Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Isiolo. Tayari mwakilishi wa papa nchini Kenya na Sudan Kusini Askofu Mkuu Hubertus Matheus Maria van Megen, pia alituma mawasiliano rasmi kwa Baraza la Maaskofu Katoliki KCCB baada ya tangazo hili la Papa Francis.

Mnamo Juni 2021 Askofu Mkuu Maria Van Megen alipokuwa akizuru Isiolo, alisema yuko kwenye misheni ya  kutathmini ukuaji wa imani katika Vikariate hiyo ili kuripoti kwa Papa Francisko na kupendekeza kile kinachohitajika kufanywa ili kuimarisha shughuli za uinjilishaji katika eneo hilo. Kazi yake pia ilikuwa kutathmini jinsi Vikariate inaweza kuboreshwa au hata kuinuliwa kuwa jimbo kamili.

Vikariate ya Isiolo ilizaliwa kutoka kwa Jimbo Katoliki la Meru tarehe 15 Desemba 1995.Jimbo Kikatoliki la Isiolo litahudumia eneo la kilomita 25,605 mraba, huku takwimu za mwaka wa 2020 zikionyesha kuwa Vikariate hiyo iliyopandishwa hadhi ilikuwa na jumla ya waumini wa kikatoliki wapatao 64,320.

February 15, 2023