Kamati ya Sheria katika Bunge la Taifa (JLAC) imeidhinisha uteuzi wa makamishna saba wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), akiwemo Erastus Edung Ethekon aliyependekezwa kuwa mwenyekiti. Katika ripoti iliyowasilishwa bungeni Jumanne, Juni 3, 2025, Mwenyekiti wa JLAC ambaye pia ni Mbunge wa Tharaka, George Murugara, alithibitisha kuwa kamati hiyo imewapitisha wagombea wote walioteuliwa na Rais William Ruto.
Ripoti hiyo sasa inasubiri kujadiliwa na Bunge lote kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa.
“Kwa kuzingatia matokeo ya kamati yetu kuhusu kuwapiga msasa walioteuliwa kuwa mwenyekiti na makamishna wa IEBC, tunapendekeza uteuzi wa Erastus Edung Ethekon kama mwenyekiti na Ann Njeri Nderitu, Moses Alutalala Mukhwana, Mary Karen Sorobit, Hassan Noor Hassan, Francis Odhiambo Aduol, na Fahima Araphat Abdallah kama makamishna wa IEBC,” alisema Murugara.
Hata hivyo, Mahakama Kuu kupitia Jaji Lawrence Mugambi ilitoa agizo la kusitisha kuchapishwa kwa majina na pia kuapishwa kwa makamishna hao hadi kesi iliyowasilishwa kupinga mchakato huo itakaposikilizwa na kuamuliwa. Jaji Mugambi alieleza kuwa masuala yaliyowasilishwa mahakamani yanahusu maslahi ya umma na yanahitaji uchunguzi wa kina wa kisheria.
“Masuala yaliyoibuliwa katika kesi hii yanahusu mamlaka ya wananchi na yanahitaji uchunguzi wa kina wa kikatiba,” alisema Jaji Mugambi.
Mchakato wa kuunda upya IEBC umekuwa ukifuatiliwa kwa karibu na wadau mbalimbali, huku baadhi ya makundi ya vijana yakilalamikia ukosefu wa uwakilishi wa vijana katika orodha ya walioteuliwa.