Kenya leo inaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya UKIMWI Duniani. Siku hii hua maalum ya kuongeza uhamasisho kuhusu UKIMWI, kutathmini mwenendo wa maambukizi. Pia hutumika kuhimiza jamii kuendeleza juhudi za kinga na matibabu.

    Kaulimbiu ya mwaka huu, “Kushinda Maambukizi, Kubadili Mwelekeo wa Kuukabili UKIMWI” inasisitiza umuhimu wa uongozi thabiti, ushirikiano wa kimataifa na mbinu zinazolinda haki za binadamu ili kufikia lengo la kumaliza UKIMWI ifikapo mwaka 2030.

    Wataalamu wa afya wanasema kuwa licha ya hatua kubwa zilizopigwa, vita dhidi ya UKIMWI bado viko katika hatua changa. Huduma za afya zimekuwa zikikumbwa na changamoto mbalimbali, huku maelfu ya watu wakiendelea kuambukizwa na wengine kupoteza maisha. Hata hivyo, mashirika ya kijamii, wahudumu wa afya na watu wanaoishi na UKIMWI wameendelea kuonyesha ustahimilivu na ubunifu, hatua inayotoa tumaini katika mapambano haya.

    Mambo Muhimu Kuhusu VVU/UKIMWI

    Ugonjwa huu tayari umesababisha vifo takribani milioni 44.1 duniani kote, na maambukizi bado yanaendelea katika nchi zote.

    Kufikia mwishoni mwa 2024, takriban milioni 40.8 walikuwa wanaishi na VVU, ambapo asilimia 65% yao wako katika Kanda ya Afrika ya WHO.

    Mwaka 2024 pekee, watu 630,000 walifariki kutokana na sababu zinazohusiana na UKIMWI, huku milioni 1.3 wakiambukizwa upya.

    Hata hivyo, kwa kutumia kinga, vipimo, matibabu na huduma sahihi, VVU imekuwa ugonjwa unaoweza kudhibitiwa. Watu wanaoishi na VVU wanaweza kuishi maisha marefu na yenye afya.

    Maelezo kutoka kwa WHO

    December 1, 2025

    Leave a Comment