magavana sukari

    Baraza la Magavana limeonyesha uungwaji mkono wake kwa mpango wa serikali ya kitaifa wa mageuzi katika sekta ya sukari, hasa hatua ya kukodisha kampuni za sukari kwa sekta binafsi. Hatua hiyo inalenga kuimarisha ufanisi wa viwanda hivyo na kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa wakulima.

    Wakizungumza mjini Mombasa katika mkutano wa pamoja na Waziri wa Kilimo Mutahi Kagwe, viongozi wa Baraza hilo—akiwemo Mwenyekiti Ahmed Abdullahi, Naibu Mwenyekiti Mutahi Kahiga, na Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo Ken Lusaka—walitoa wito kwa wadau wote kuunga mkono mchakato huo. Viongozi hao walisema kuwa mageuzi hayo ni ya lazima ili kufufua sekta ya sukari ambayo imekuwa ikikumbwa na changamoto kwa miaka mingi.

    Mwenyekiti Abdullahi alisisitiza kuwa siasa hazipaswi kuingizwa katika mchakato huo, kwani lengo kuu ni kuinua maisha ya wakulima na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika maeneo yanayolima miwa.

    Kwa upande wake, Waziri Mutahi Kagwe alieleza kuwa serikali imechukua hatua ya kukodisha kampuni nne kuu za sukari kwa kipindi cha miaka 30, akisema mpango huo utaongeza tija, kuboresha huduma, na kuwanufaisha wakulima kupitia malipo bora na huduma za usimamizi zenye ufanisi zaidi.

    Mpango huu wa mageuzi unajiri wakati baadhi ya wakulima na viongozi wa maeneo yanayolima miwa wakieleza wasiwasi kuhusu ushirikishwaji wao katika mchakato huu. wakulima kutoka kaunti za Kisumu na Nandi wameelezea malalamiko kuhusu namna zoezi hilo lilivyotekelezwa, wakidai kuwa hawakuhusishwa kikamilifu katika hatua mbalimbali za mchakato huo. Wakulima hao wamesema tayari wamewasilisha kesi mahakamani wakitaka zoezi hilo kusitishwa hadi pale ambapo watahusishwa ipasavyo.

    May 16, 2025

    Leave a Reply