Kinshasa, DRC – Mahakama Kuu ya Kijeshi mjini Kinshasa imemhukumu kifo aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Joseph Kabila, aliyepatikana na hatia ya uhaini, uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Uamuzi huo ulitangazwa Jumanne, katika kesi hiyo iliyoua imeahirishwa mara kadhaa. Mahakama ilisikiliza ombi la upande wa mashtaka ulioongozwa na Mwendesha Mashtaka Mkuu, Lucien René Likulia. Likulia alisisitiza kuwa Kabila alihusika kupanga mashambulizi ya waasi wa AFC/M23 mashariki mwa Kongo.
Kesi ilihusisha tuhuma za mauaji, ubakaji, mateso na uhamisho wa raia. Aidha, Mahakama iliagiza kufungia mali za Kabila na kumlazimisha kulipa zaidi ya dola bilioni 24 kama fidia kwa waathirika.
Hata hivyo, Kabila alikana mashtaka na kuyaita “ya kisiasa”. Pia alisisitiza hana uhusiano wowote na waasi wa M23. Kwa kuwa hakuhudhuria kikao, hukumu imetolewa kwa kificho (in absentia).
Kiongozi huyo wa zamani, mwenye umri wa miaka 54, aliiongoza DRC kwa miaka 18. Aliingia madarakani mwaka 2001 baada ya kuuawa kwa baba yake, Laurent Kabila. Mnamo mwaka 2019 alimkabidhi madaraka Rais wa sasa Félix Tshisekedi. Baada ya tofauti zao kisiasa, Kabila aliondoka nchini mwaka 2023. Hata hivyo, alirejea Mei 2025 baada ya Seneti kumvua kinga ya kisheria, hatua iliyopelekea mashtaka kuendelea.
Kesi hii inachukuliwa kuwa hatua ya kihistoria katika mfumo wa sheria wa Kongo. Hata hivyo, wafuasi wa Kabila wanaiona kama njama ya kisiasa ya kumzuia kurejea kwenye ulingo wa siasa.
Kwa sasa, mashariki mwa DRC bado inakabiliwa na mapigano makali. Waasi wa M23 wanadhibiti maeneo muhimu yenye utajiri wa madini. Aidha, Rwanda imetuhumiwa na Umoja wa Mataifa na mataifa ya Magharibi kwa kuunga mkono waasi hao, madai ambayo Kigali imekanusha.