Spika wa Bunge la Taifa, Moses Wetang’ula, amethibitisha kupokea rasmi rasimu ya Mswada wa Fedha wa mwaka 2025, saa chache baada ya kuidhinishwa na Baraza la Mawaziri katika kikao kilichoongozwa na Rais William Ruto, Jumanne hii.
Spika Wetang’ula alieleza kuwa mswada huo utapelekwa kwa Kamati ya Bunge ya Fedha na Mipango ya Kitaifa kwa ajili ya kuupitia na kuratibu ushirikishwaji wa umma, mara tu baada ya kusomwa kwa mara ya kwanza bungeni.
“Ninapenda kulifahamisha Bunge kuwa nimepokea rasmi Mswada wa Fedha 2025 kutoka kwa Baraza la Mawaziri. Mswada huu unahusiana na mbinu za serikali za kuongeza mapato kwa ajili ya bajeti iliyowasilishwa,” alisema Spika Wetang’ula.
Aidha, aliwasihi wabunge kusoma na kufahamu kwa kina yaliyomo kwenye mswada huo ili kuhakikisha maoni yao na ya wapiga kura wao yanazingatiwa wakati wa mchakato wa kuupitia.
Serikali kupitia taarifa ya Baraza la Mawaziri imeeleza kuwa lengo kuu la mswada huu si kuongeza ushuru bali kuziba mianya ya upotevu wa mapato, kuongeza ufanisi wa kiutawala, na kupunguza ukwepaji ushuru. Mabadiliko yaliyopendekezwa ni pamoja na kurahisisha urejeshwaji wa ushuru, kuboresha sheria za usuluhishi wa mizozo ya ushuru, na kuruhusu biashara ndogo kukata gharama za vifaa kamili ndani ya mwaka wa ununuzi.
Hata hivyo, Wabunge wametahadharishwa dhidi ya taarifa potofu zinazosambaa mitandaoni kuhusu mswada huo. Mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohamed, alisema kuwa baadhi ya Wakenya wamekuwa wakijadili toleo ghushi la mswada huo.
“Tunawaomba Wakenya kutegemea nakala halisi ya Mswada wa Fedha iliyowasilishwa bungeni. Hakuna ushuru mpya ulioongezwa kama inavyodaiwa mitandaoni. Tuwaeleze wananchi ukweli,” alisema Junet.
Wabunge wamesisitizwa kueneza taarifa sahihi kwa wananchi kuhusu mswada huo huku ukisubiriwa kusomwa kwa mara ya kwanza na kufunguliwa kwa maoni ya umma.