Haiti

Serikali ya Marekani imetangaza kusitisha ufadhili wake kwa operesheni ya Umoja wa Mataifa inayolenga kurejesha utulivu nchini Haiti. Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza kuwa ufadhili wa Shilingi bilioni 1.71 (Dola milioni 13.3) utasitishwa mara moja.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric, amethibitisha kupokea notisi rasmi ya kusitishwa kwa ufadhili huo. Operesheni hiyo inayoendelea nchini Haiti inaongozwa na maafisa wa Kenya wanaokabiliana na magenge ya wahalifu.

Uamuzi wa kusitisha ufadhili huo ni sehemu ya mpango wa Trump wa kupunguza misaada ya kigeni, ikiwemo kufunga baadhi ya shughuli za USAID. Haiti kwa sasa haina rais wala bunge na inatawaliwa na viongozi wa mpito.

Zaidi ya watu 5,626 waliuawa nchini humo mwaka jana kutokana na ghasia za magenge, idadi hiyo ikiwa takriban elfu moja zaidi ya mwaka 2023, Umoja wa Mataifa ulisema.

Zaidi ya raia milioni moja wa taifa hilo wamelazimika kukimbia makazi yao, idadi hiyo ikiwa mara tatu zaidi ya mwaka mmoja uliopita. Hali nchini Haiti inaendelea kuwa tete, huku magenge ya wahalifu yakiendeleza unyanyasaji dhidi ya wananchi.

SOMA PIA: Rais Ruto na Waziri Mkuu Ariel Henry wajadili Usaidizi wa Kurejesha Amani Haiti.

February 5, 2025