Seneti

Maseneta nchini wameshtumu mawaziri watatu, akiwemo Waziri wa Mahusiano ya Nje, Alfred Mutua, Waziri wa Afya, Susan Nakhumicha, na Waziri wa Leba, Florence Bore, baada yao kukataa kujiwasilisha katika vikao vya bunge hilo. Lengo la kujiwasilisha kwao lilikuwa ni kutoa taarifa na kujibu maswali kuhusu utendakazi wao.

Spika wa Bunge la Seneti Amason Kingi ameeleza kusikitishwa na hulka ya mawaziri hao, akisisitiza kwamba ni jukumu lao kuhudhuria vikao vya bunge na kutoa taarifa zinazohitajika na wawakilishi wa umma. Seneta wa Nandi Samson Cherargei amekosoa vikali uamuzi wa watatu hao, huku akibainisha kwamba vikao vya bunge vinatekeleza wajibu wa wawakilishi wa Wakenya, hivyo wote wanaoitwa bungeni wana Jukumu la kujiwasilisha.

Miongoni mwa mawaziri hao watatu, Waziri wa Leba, Florence Bore, alitoa taarifa ya kutokuhudhuria kwake, akieleza kuwa yuko katika ziara ya kikazi nchini Tanzania, ambapo anaandamana na Rais Ruto kwenye shughuli za kitaifa. Sheria za Seneti zinawaongoza wote walioalikwa kwenye vikao katika bunge hilo, kutoa taarifa mapema iwapo hawataweza kufika, ili kuruhusu mipango kabambe kuwekwa.

 

July 26, 2023