BY ISAYA BURUGU 23RD DEC  2022-Baraza la Vyombo vya Habari nchini Kenya limeomba Huduma ya Kitaifa ya Polisi kuharakisha uchunguzi kuhusu mauaji ya mwanahabari Moses Okiror Omusolo.

Baraza hilo limelaani mauaji ya kutisha ya Omusolo, likisema kuwa usalama wa wanahabari ni muhimu.

“Huduma ya Kitaifa ya Polisi inahitaji kufanya uchunguzi wa haraka kuhusu kitendo hicho kiovu na hatua zinazofaa kuchukuliwa dhidi ya wahalifu,” walisema kwenye taarifa kwenye Twitter.

Omusolo alikuwa mwanahabari wa biashara katika Standard Group kabla ya maisha yake kukatizwa.

Alipatikana akiwa ametupwa, amekufa kwenye mtaro kando ya Barabara ya Kang’undo, Nairobi mnamo Alhamisi.

Polisi walisema wanashuku kuwa aliuawa kwingine na mwili huo kutupwa katika eneo hilo.

Wenyeji waliripoti kwa polisi kulikuwa na mwili ukiwa kando ya barabara mkabala na Kampuni ya Superloaf.

Polisi walisema walitembelea eneo la tukio na kubaini Omusolo alikuwa na mkato mkubwa upande wa kulia wa kichwa huku damu ikivuja.

Polisi walisema bado hawajajua nia ya mauaji hayo.

December 23, 2022