Mgomo wa wahadhiri katika Chuo Kikuu cha Moi, Eldoret, unaendelea huku mazungumzo kati ya Muungano wa Wahadhiri wa Vyuo Vikuu (UASU) na usimamizi wa chuo hicho yakiendelea bila mwafaka.
Katibu Mkuu wa UASU tawi la Eldoret, Busolo Wekesa, amesema mgomo utaendelea hadi pale usimamizi wa chuo utakapowapa wanachama masharti bora. Mazungumzo yalianza Alhamisi, siku moja baada ya mgomo kuanza, lakini bado hayajazaa matunda.
Wahadhiri waligoma rasmi tarehe 20 Agosti 2025 baada ya kutoa ilani ya siku saba. Walidai walipwe mishahara ya miezi ya Juni na Julai 2025 kwa viwango vilivyokubaliwa kwenye mkataba wa pamoja wa 2021–2025.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa kitaifa wa UASU, Constatine Wasonga, amesisitiza kwamba mgomo utaendelea hadi masharti ya makubaliano ya 30 Novemba 2024 yatakapotekelezwa kikamilifu. Makubaliano hayo yalihusu malipo ya mishahara, kupandishwa vyeo, na umri wa kustaafu.
“Hadi pale Return-To-Work Formula itakapotekelezwa kikamilifu, wanachama wote wa UASU katika Moi University wamesitisha kazi,” alisema Wasonga.
Aidha, Wekesa amesema wanachama bado wanapitia mapendekezo mapya ya usimamizi kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho. Hata hivyo, alisisitiza kwamba mgomo utaendelea kwa sasa.