Kamati ya usalama katika kaunti ya Narok inatarajiwa kuzuru msitu wa Mau siku ya Jumatano 12,Oktoba 2022, kwa ziara ya kiusalama katika msitu huo. Kamishena wa Kaunti ya Narok Bw. Isaac Masinde, amesema kuwa kamati hiyo itatumia ndege kupaa juu ya msitu huo wakati wa ziara hiyo, inayopania kuhakikisha kuwa msitu huo uko salama. Kamishena huyo ambaye amesisitiza kujitolea kwa serikali katika kuhifadhi msitu huo, ametoa onyo kali kwa watu walio na nia ya kuendeleza shughuli zozote zilizopigwa marufuku katika msitu huo kama vile ukulima na kuwapeleka mifugo msituni humo akieleza kuwa hawatasita kuwachukulia hatua wahusika wote.

Msitu wa Mau umekuwa kiungo muhimu katika taifa la Kenya, wanasiasa wakionekana kutumia msitu huo kama chombo cha kujitafutia uungwaji mkono kwenye harakati zao za siasa, mara kwa mara wakiwaahidi wananchi uwa wataufungu msitu huo ili kuwapa makaazi na mashamba pamoja na chakula kwa mifugo wao, jambo ambalo kamishena masinde amelipinga nakuahidi kuwaadhibu wote wataoendeleza shughuli kama hizo.

Kaunti ya Narok ni Kaunti ambayo inategemea utalii, bila mto Mara, hata utalii utaenda chini, kwa hivyo lazima tuilinde chemichemi ya maji ya mto huu kwa njia zozote zile.

Zaidi ya hayo kamishena Masinde amesisitiza umuhimu wa msitu huu katika ukuaji wa kaunti ya Narok, akitaja uhusiano wake na Mbuga ya Maasai Mara ambayo huwa kitega uchumi kikubwa zaidi katika kaunti ya Narok. Kwa maneno yake Bw. Masinde, iwapo Mto Mara utashuhudia uhaba wa maji kutokana na kudhiriwa kwa msitu wa Mau, huenda idadi ya watalii wanaomiminika katika kaunti ya Narok ikapungua, jambo ambalo litaathiri kipato katika kaunti ya Narok.

October 6, 2022