Mwanume Kunajisi

    Mahakama ya Kabarnet imemhukumu mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 42 kutoka kijiji cha Bepyemit, Kaunti ya Baringo, kifungo cha miaka 15 gerezani kwa kosa la kumnajisi binti yake mwenye umri wa miaka 8.

    Kulingana na taarifa kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP), mshtakiwa ambaye ni baba mzazi wa mtoto huyo, alitekeleza ukatili huo mara kadhaa mwaka jana alipokuwa akimtembelea mkewe.

    Mahakama iliambiwa kuwa mshtakiwa alikuwa na mazoea ya kumdanganya mtoto huyo kabla ya kutenda kitendo hicho cha kinyama. Upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi sita, wakiwemo wataalamu wa afya, pamoja na ushahidi wa kitabibu na ripoti ya uchunguzi iliyothibitisha kuwa mshtakiwa alihusika moja kwa moja.

    Akitoa hukumu, Hakimu Purity Koskey alieleza kusikitishwa sana na tukio hilo, akikitaja kuwa ni tendo la kikatili lisilostahili kuvumiliwa katika jamii yoyote. Alisisitiza umuhimu wa kulinda haki za watoto na kuwahakikishia wahalifu wa aina hiyo kuwa sheria itachukua mkondo wake ipasavyo.

    June 4, 2025