ngugi wa thiong'o

    Mwandishi mashuhuri wa Kenya, msomi na mwanaharakati Ngũgĩ wa Thiong’o amefariki dunia Jumatano jioni, Mei 28, 2025, akiwa na umri wa miaka 87.

    Familia yake ilitangaza kifo chake na kueleza kuwa aliishi maisha yake kikamilifu huku kamili huku wakihimiza watu waliomjua kusherehekea maisha na mchango wake wa kipekee katika jamii na fasihi.

    Ngũgĩ alikuwa na mchango mkubwa katika fasihi ya Kiafrika, ambapo kazi zake zilivuka mipaka ya lugha, mabara na vizazi. Baadhi ya kazi zake maarufu ni pamoja na A Grain of Wheat, The River Between, Petals of Blood, Weep Not Child, na Devil on the Cross.

    Alizaliwa mwaka 1937 katika kijiji cha Kamiriithu, Limuru, na maisha yake ya uandishi yalifungamana kwa karibu na harakati za uhuru wa Kenya pamoja na utambulisho wa baada ya ukoloni.

    Picha ya baadhi ya vitabu ambavyo vimeandikwa na Ngũgĩ wa Thiong’o

    Mwaka 1977, tamthilia yake maarufu Ngaahika Ndeenda, iliyochezwa kwa lugha ya Gikuyu, ilisababisha kukamatwa kwake na kuzuiliwa bila mashtaka chini ya utawala wa Daniel arap Moi. Tukio hilo lilikuwa ni hatua ya mabadiliko katika maisha yake ya kitaaluma, ambapo aliacha kuandika kwa Kiingereza na kuanza kutumia Gikuyu, kisha kutafsiri kazi zake kwa lugha nyinginezo.

    Kwa miongo kadhaa, Ngũgĩ aliishi uhamishoni huku akifundisha katika vyuo vikuu vikuu duniani, ikiwemo Yale na Chuo Kikuu cha California, Irvine.

    Licha ya kuwa mbali na nyumbani, aliendelea kuwa na uhusiano wa karibu na Kenya kupitia lugha yake, uharakati, na msimamo mkali dhidi ya dhuluma.

    Kutoka kila kona ya dunia, heshima na salamu za rambirambi zimeanza kumiminika, zikimkumbuka Ngũgĩ si tu kama gwiji wa fasihi, bali pia kama mtetezi wa haki na uhuru wa fikra.

    May 28, 2025

    Leave a Comment