Rais William Ruto amepongeza ukomavu wa wakenya katika kuangazia maswala muhimu ya taifa, na kwa kujiepusha na ukabila pamoja na misingi ya kijamii katika kujadili maswala haya.

Akihutubia taifa katika maadhimisho ya Madaraka huko Embu, Rais ameeleza kuridhishwa na gumzo kuhusiana na mswada wa fedha pamoja na mpango wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu kote nchini, akisema mazungumzo ya aina hii yatawezesha taifa kupiga hatua mbele kimaendeleo na kutoa mwongozo unaofaa kwa wakenya kuhusu ajenda za serikali.

Aidha aliendelea kuupigia debe mpango wake wa ujenzi wa nyumba kwa wakenya, akieleza kwamba hii ni mojawapo ya njia za kuinua hadhi ya maisha ya wakenya.

Katika hotuba yake vilevile, Rais amesema kwamba wafanyakazi katika sekta ya bodaboda nchini watanufaika na mpango wa kupata pikipiki zinazotumia nguvu za umeme kuanzia mwezi Septemba mwaka huu. Ruto alieleza kwamba serikali yake iko tayari kukuza sekta hii, kwa kuwapeusha na unyanyasaji kutoka kwa wauzaji wa pikipiki hizi kwa mikopo, na badala yake kuwawezesha kupata huduma zao kwa njia ya kuwajali.

June 1, 2023