Sabina Chege na Mark Mwenje

Mbunge wa Embakasi Magharibi, Mark Mwenje, ameidhinishwa kuwa Naibu Mnadhimu wa Wachache katika Bunge la Taifa, akichukua wadhifa huo kutoka kwa Mbunge Mteule Sabina Chege.

Uamuzi huu ulitangazwa rasmi na Spika wa Bunge, Moses Wetangula, baada ya kesi iliyokuwa inazuia mabadiliko katika uongozi wa nyadhifa za bunge katika muungano wa Azimio la Umoja kufutiliwa mbali na mahakama.

Katika taarifa yake kwa wabunge wakati wa kikao cha adhuhuri, Spika Wetangula alieleza kwamba kila chama cha kisiasa kina uwezo wa kikatiba kufanya mabadiliko katika uongozi wake katika bunge. Hivyo basi, uamuzi wa kumuidhinisha Mark Mwenje kuwa Naibu Mnadhimu wa Wachache ulikuwa kwa mujibu wa taratibu za muungano wa Azimio la Umoja.


Katika tangazo hilo vilevile, Spika Wetangula alitangaza kwamba Chama cha Jubilee kimepewa kibali cha kuendeleza shughuli zake katika Bunge la Taifa kama chama huru cha kisiasa huku mbunge Mteule Sabina Chege akipewa jukumu la kuwa Mnadhimu wa Chama hicho kwa muda. Chege ambaye alipigiwa kura na wabunge wa chama hicho kuwa mmoja wa viongozi katika chama chenyewe atahudumu kikaumu huku uamuzi mwingine ukitarajiwa kutolewa kuhusu uongozi wa chama hicho.

 

Share the love
October 25, 2023