Sanae Takaichi, ameandika historia baada ya kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke wa Japan.
Takaichi (64) alivuna kura 237 katika Baraza la Wawakilishi na 125 katika Baraza la Wajumbe.
Uongozi Mpya Wakati wa Changamoto
Takaichi, ambaye ni mfuasi wa sera za kihafidhina, anachukua uongozi wakati ambapo Japani inakabiliwa na gharama kubwa ya maisha na wananchi waliokata tamaa.
Hii ni mara ya nne kwa Japan kubadilisha Waziri Mkuu ndani ya miaka mitano, baada ya watangulizi wake kuondoka kutokana na kashfa na kushuka kwa uungwaji mkono.
Msaada wa Kisaasa Kisiasa
Awali, ilionekana kama Takaichi angepoteza nafasi hiyo baada ya chama mshirika Komeito kujiondoa.
Lakini makubaliano ya dakika za mwisho na chama cha Japan Innovation Party (JIP) yaliokoa kampeni yake na kumpa uongozi. Atakabiliwa na uchaguzi mkuu mwaka 2028.
Mahusiano ya Kimataifa
Takaichi anakabiliwa na mtihani katika uhusiano wa kimataifa. Korea Kusini imeonyesha wasiwasi kutokana na siasa zake za mrengo wa kulia, zinazoshabihiana na za aliyekuwa waziri mkuu Shinzo Abe.
Pia, anaonekana kuwa mkali dhidi ya China, huku akijiandaa kwa kikao cha kwanza na Rais wa Marekani Donald Trump wiki ijayo.
Ingawa mataifa hayo mawili yamekubaliana kuhusu ushuru, kauli za Trump kuhusu mkataba wa usalama na gharama za ulinzi zinaibua wasiwasi. Takaichi atalazimika kuongoza mazungumzo kwa uangalifu.
Safari ya Kisiasa ya Takaichi
Takaichi ni mwandani wa marehemu Shinzo Abe na ameshika nyadhifa kadhaa serikalini.
Aliwania urais wa chama cha Liberal Democratic Party (LDP) mara kadhaa kabla ya kushinda mwaka huu, baada ya Shigeru Ishiba kujiuzulu kufuatia kushindwa vibaya katika uchaguzi wa kati. Anajulikana kama “Iron Lady” wa Japani kwa kufuata nyayo za Margaret Thatcher. Anapinga ndoa za jinsia moja na pendekezo la wanawake walioolewa kubaki na majina yao ya awali.
Mipango Yake ya Kijamii
Katika kampeni yake, Takaichi alipendekeza kuimarisha huduma za afya kwa wanawake na kutoa hadhi zaidi kwa wafanyakazi wa nyumbani.
Anakabiliwa na jukumu kubwa la kujenga upya imani ya wananchi kwa chama chake, LDP, ambacho kimeongoza Japan kwa miaka mingi lakini kimepoteza umaarufu kutokana na kashfa za ufadhili.
Changamoto za Kiuchumi
Takaichi anakabiliwa na gharama kubwa za maisha na ukosefu wa mpunga ambao umepelekea bei kupanda.
Vyombo vya habari vya Japan vimeripoti kuwa huenda akamteua Satsuki Katayama kuwa Waziri wa Fedha — hatua ambayo pia itakuwa ya kihistoria kwa mwanamke mwingine.
Licha ya wasiwasi kuhusu deni la taifa na ukuaji mdogo wa uchumi, ushindi wa Takaichi umeleta matumaini mapya sokoni.