BY ISAYA BURUGU 30TH DEC 2022-Mtangazaji mkongwe wa runinga Catherine Kasavuli ameaga dunia.Alifariki akiwa na umri wa miaka 60 katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta Alhamisi usiku, baada ya kuugua saratani.Kasavuli amelazwa katika hospitali hiyo tangu Oktoba 26.

Mfanyakazi mwenzake katika KBC aliwafahamisha Wakenya kuhusu hali yake.Mwezi mmoja uliopita Kasavuli alihitaji damu akiwa amelazwa katika hospitali hiyo baada ya hali yake kuwa tete ambapo kwa muda amekuwa akipigana vita ugonjwa wa saratani ya kizazi.

Mkurugenzi Mkuu wa KBC Samuel Maina alithibitisha kifo cha mwanahabari huyo asubuhi ya Ijumaa akisema alikata roho Alhamisi usiku.Mwanahabari huyo maarufu alistaafu kutoka utangazaji wa runinga mnamo 2013 baada ya kazi ndefu na iliyopambwa katika tasnia ya habari kama mtangazaji wa habari.

Kasavuli alianza kazi ya utangazaji miaka ya 80 ambapo pia alikuwa mwanahabari wa kwanza kupeperusha habari mubashara katika runinga ya KTN ilipozinduliwa mwishoni mwa miaka ya 80.Baada ya kustaafu kutoka runingani 2013, mwaka jana KBC walimuajiri tena kuwa kinara wa kipindi Cha wakongwe waliovuma katika tasnia mbalimbali enzi hizo.

Kasavuli alikuwa amepumzika kwa miezi minne na akarejea kwenye mtandao wake wa Instagram mnamo Oktoba.Mnamo Novemba, wafanyakazi wenzake na marafiki katika tasnia ya habari walianzisha kampeni kumchangia damu akiwa KNH.

 

December 30, 2022