Wabunge wa chama cha ODM wamekashifu vikali taarifa za polisi kuhusu kifo cha mwanablogu Albert Ojwang, ambaye alifariki akiwa katika himaya ya polisi katika Kituo cha Polisi cha Central jijini Nairobi. Katika taarifa yao, polisi wamedai kuwa Ojwang alijitoa uhai, lakini wabunge hao wamesema madai hayo hayaendani na ushahidi uliopo.
Kwa mujibu wa wabunge hao, mazingira ya kifo hicho yanahitaji kuchunguzwa kwa uwazi. Wametaka Tume ya IPOA, Tume ya KNCHR na taasisi nyingine huru zichukue hatua mara moja ili kuhakikisha haki inatendeka.
Aidha, wamemkumbusha Rais William Ruto kuhusu ahadi yake ya awali ya kuhakikisha hakuna raia anayepoteza maisha mikononi mwa maafisa wa usalama. Wamesisitiza kuwa familia ya Albert Ojwang inahitaji haki, na wote waliohusika wanapaswa kuwajibishwa ipasavyo.
Kwa upande mwingine, Baraza la Magavana pia limeungana na wito huo. Mwenyekiti wa baraza hilo, Ahmed Abdulahi, amelilaani tukio hilo na kulitaja kuwa la kusikitisha. Amesema tukio hilo linaonyesha kuwa kuna dosari kubwa katika utekelezaji wa sheria na haki nchini.
Baraza hilo limesema kuwa maisha ya binadamu ni ya thamani kubwa na hayapaswi kupuuzwa. Magavana wanaitaka IPOA iharakishe uchunguzi na kutoa majibu ya haraka kwa familia ya marehemu.
Gavana wa Kakamega, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha kwenye baraza hilo, Fernandes Barasa, ameeleza kughadhabishwa kwake na kifo hicho, akieleza kuwa familia ya Ojwang inastahili kufahamu ukweli kamili kuhusu kilichotokea.