Familia za watu 21 waliopoteza maisha yao katika shambulizi la kigaidi la Dusit D2 jijini Nairobi mnamo mwaka wa 2019 sasa wamepata nafuu ya haki baada ya washukiwa wawili wa shambulizi hilo kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 gerezani kila mmoja.
Katika uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu jijini Nairobi siku ya Alhamisi, Jaji Diana Kavedza aliwahukumu Mohammed Abdi Ali mwenye umri wa miaka 61 na Hussein Abdile Ali mwenye umri wa miaka 22 baada ya kupatikana na hatia ya kupanga na kufadhili shughuli za kigaidi zilizohusishwa na kundi la Al-Shabaab.
๐๐๐ ๐ฌ๐๐๐ฎ๐ซ๐๐ฌ ๐๐-๐ฒ๐๐๐ซ ๐ฌ๐๐ง๐ญ๐๐ง๐๐ ๐๐จ๐ซ ๐ญ๐ก๐ ๐๐ฎ๐ฌ๐ข๐ญ ๐๐ ๐ญ๐๐ซ๐ซ๐จ๐ซ ๐๐ญ๐ญ๐๐๐ค ๐๐จ๐ง๐ฏ๐ข๐๐ญ๐ฌ
The Kahawa Anti-Terror Court has sentenced a 61-year-old madrassa teacher to 30 yearsโ imprisonment for facilitating a terrorist attack at the Dusit D2โฆ pic.twitter.com/rI6YdN7Rpu
โ Office of The Director Of Public Prosecutions (@ODPP_KE) June 19, 2025
Kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama, ushahidi uliowasilishwa uliweza kuthibitisha kuwa washukiwa walishirikiana kwa karibu na washambulizi waliotekeleza shambulizi hilo lililochukua zaidi ya saa 20, ambapo watu 21 waliuawa, wengine kadhaa kujeruhiwa, na mali kuharibiwa.
Jaji Kavedza alieleza kuwa vitendo vya ugaidi ni tishio kubwa kwa usalama wa taifa na haki ya kuishi kwa kila raia, na kwa hivyo adhabu hiyo ni onyo kwa wale wanaopanga ama kufadhili vitendo vya kigaidi. Aliongeza kuwa licha ya hukumu hiyo kutoweza kufuta maumivu ya waliopoteza wapendwa wao, ni hatua muhimu ya kuhakikisha haki inatendeka na ya kuwatia moyo manusura pamoja na familia za waathiriwa.
Familia nyingi zilizokuwa mahakamani wakati wa hukumu hiyo zilionekana kuguswa na hatua hiyo ya mahakama, zikiitaja kama mwanzo wa uponyaji wa kisaikolojia baada ya miaka ya maumivu na kusubiri haki.