Seneta wa kaunti ya Kakamega Dkt. Boni Khalwale amewaonya wawakilishi wadi dhidi ya kutumia vibaya mamlaka yao ya kikatiba, kwa kuwatisha magavana ili kukidhi maslahi yao ya kibinafsi.

Khalwale ambaye alikua mwenyekiti wa kamati ya seneti iliyosikiliza hoja ya kumbandua gavana wa Meru Kawira Mwangaza, amesema kuwa wawakilishi wadi wanahitaji kuyajua majukumu yao ya msingi na kuwatumikia wakenya badala ya kuwatishia magavana kutumikia maswala ya kibinafsi.Khalwale aliyasema haya siku ya Jumatatu, alipohudhuria Sherehe ya kitamaduni ya Batsotso katika Kituo cha Eshisiru katika kaunti ya Kakamega.

Seneta Khalwale pia ameahidi kuwa bunge la seneti litatumia uwezo wake kuwatetea magavana dhidi ya wawakilishi wadi wenye ubinafsi, akiongeza kwamba uwezo wa seneti kuwabandua magavana huwa unajikita katika maswala ya utendakazi na kimaadili, kabla ya kuafikia uamuzi wa kuidhinisha kubanduliwa mamlakani kwa gavana yeyote.

January 3, 2023