Wazee Narok

Baraza la Wazee wa Jamii ya Maa nchini limetoa wito kwa Rais Dkt. William Ruto kuzindua rasmi shughuli za ukarabati wa barabara mbovu katika Kaunti ya Narok wakati atakapoanza ziara yake rasmi katika kaunti hii siku ya kesho.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa baraza hilo, Keleina Ole Nchoe, sehemu nyingi za Kaunti ya Narok zimeendelea kukumbwa na changamoto za miundomsingi duni, hasa barabara, hali ambayo imetatiza shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa maeneo husika.

Baraza hilo limebainisha kuwa maeneo ya Narok Mashariki, Narok Kaskazini, Narok Kusini na sehemu mbalimbali za Transmara Magharibi, Kusini na Mashariki yameathirika zaidi na hali mbaya ya barabara, na limehimiza kuwekwa kwa mipango ya haraka ya kuboresha mawasiliano ya barabara ili kuunganisha maeneo ya mashinani na kuboresha maisha ya wananchi.

Viongozi wa baraza hilo wamesema kuwa jamii ya Maa iko tayari kusimama imara kutetea haki zake za kimaendeleo, na kwamba sasa ni wakati muafaka kwa serikali kuzingatia mahitaji ya wakazi wa Narok kama ilivyo kwa maeneo mengine ya nchi.

Naibu Mwenyekiti wa baraza hilo, Sironga Ole Iree, ameongeza kuwa jamii ya Maa inaendelea kuunga mkono serikali ya Rais Ruto na ipo tayari kumpokea rais kwa heshima katika ziara yake ya kesho, kwa matumaini kwamba kero za wananchi zitasikika na kushughulikiwa ipasavyo.

May 5, 2025

Leave a Reply