Baadhi ya Wakaazi wa mtaa wa majengo mjini Narok wameelezea wasiwasi wao kuhusu hali ya usafi katika maeneo ya makaazi, wakitoa wito kwa wakaazi wenzao na serikali ya kaunti kuchukua hatua za dharura ili kuboresha mazingira na afya ya jamii.
Wakizungumza na wanahabari wa radio Osotua wakaazi hao wamesema kuwa hulka ya baadhi ya watu wanaoishi kwenye nyumba za kukodisha kutupa taka ovyo na kumwaga maji machafu karibu na maakazi yao, ni chanzo kikuu cha uchafuzi wa mazingira hali wanayosema imesababisha mitaa mingi kujaa takataka zinazochangia uvundo.
Hali kadhalika wametoa ombi kwa serikali ya kaunti ya Narok kupitia idara ya mazingira kuweka mapipa ya takataka katika maeneo ya makaazi sawa na kusafisha mitaro ya kupitisha majitaka mara kwa mara ili kuzuia maambukizi ya magonjwa.