Wananchi katika eneo la Majengo mjini Narok wamelalamikia ukosefu wa huduma za taa za barabarani kwa muda sasa, hali wanayosema inahatarisha usalama wao na kuathiri shughuli za kibiashara, hasa kwa wachuuzi wanaofanya kazi hadi usiku.
Wakazi hao wamesema kuwa kwa kipindi kirefu taa hizo zimekuwa hazifanyi kazi, jambo ambalo limepelekea kuongezeka kwa visa vya uhalifu eneo hilo. Baadhi yao wameeleza kuwa giza nene linalokuwepo wakati wa asubuhi na jioni limewafanya kuogopa kuwaruhusu watoto wao kwenda shule mapema kwa kuhofia usalama wao.
“Tuko na shida ya giza, hata tunaibiwa sana nyakati za usiku. Tunaomba hii stima irudishwe juu kwenye hii njia, tunateseka zaidi,” alisema mmoja wa wachuuzi katika eneo hilo.
Mfanyabiashara mwingine anayeuza mboga alisema wamelazimika kufunga biashara zao mapema kwa kuhofia usalama wao na kutokana na hasara wanazopata baada ya kuibiwa bidhaa zao.
Wananchi sasa wanatoa wito kwa asasi husika kuhakikisha kuwa taa za barabarani katika eneo hilo zinarejeshwa ili kuimarisha usalama na kuwezesha shughuli za kiuchumi kuendelea bila hofu.