Waziri wa Ardhi Alice Wahome amesema usajili wa shamba la Olkiombo lenye ekari 4,700 lililoko ndani ya Hifadhi ya Wanyama ya Maasai Mara ulifanywa bila kufuata taratibu za kisheria.
Akizungumza mbele ya Kamati ya Ardhi ya Bunge, Waziri alisema hakuna ushahidi wa upimaji wa shamba hilo kabla ya hati ya umiliki kutolewa. Ardhi hiyo, ambayo kwa sasa inamilikiwa na Livingston Kunini Ntutu, ndugu wa Gavana wa Narok Patrick Ole Ntutu, imekuwa chanzo cha mgogoro wa muda mrefu.
Mgogoro wa Olkiombo umedumu kwa takriban miaka 30, ukihusisha sehemu ya jamii ya Kimaasai na familia ya Ntutu. Mapema mwaka huu, Mahakama ilimkabidhi Kunini hati ya umiliki, lakini hatua hiyo ilizua ghasia na malalamiko kutoka kwa wakazi wa eneo hilo.
Kwa sasa, suala hilo limefikishwa katika Mahakama ya Rufaa baada ya ushahidi mpya kufichuliwa bungeni. Wabunge wameibua maswali zaidi kuhusu uhalali wa nyaraka za ardhi, wakisema hakuna rekodi rasmi zinazothibitisha usajili wa shamba hilo.