Waziri wa Nishati na Petroli (CS) Opiyo Wandayi amesisitiza kwamba Kenya ina akiba ya kutosha ya bidhaa za petroli huku akiwarai wakenya kutokuwa na hofu.
Akihutubia waandishi wa habari Wandayi amesema kwamba mnyororo wa usambazaji uko sawa na akiba ya mafuta ya Kenya iko katika kiwango kinachohitajika.
Kulingana naye, Kampuni ya usafirishaji mafuta nchini inashikilia lita milioni 102 za Petroli, lita milioni 146 za Dizeli, lita milioni 157 ya Mafuta ya Taa.
Alisema kwamba meli ya dizeli kwa sasa inamwaga mafuta katika bandari ya Mombasa, na meli zaidi zinatarajiwa kumwaga lita milioni 288.Aidha alionya kampuni za uuzaji wa mafuta zinazohifadhi mafuta.
Alizidi kuwarai Wakenya kutonunua petroli kwa wingi akiwahimiza kuwa watulivu na kuendelea na mifumo yao ya kawaida ya ununuzi.
Ikiwa kuna haja ya kubadilisha bei, aliongeza, serikali itatoa taarifa yake rasmi kupitia EPRA, lakini kwa sasa, Wakenya wanapaswa kuendelea kupokea usambazaji usiokatizwa wa bidhaa za petroli.

